1. Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu;
2. ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang’anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao!
3. Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi?
4. Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.
5. Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu!
6. Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani.
7. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache.
8. Maana asema, Je! Wakuu wangu si wote wafalme?
9. Je! Kalno si kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi? Samaria si kama Dameski?
10. Kama vile mkono wangu ulivyofikilia falme za sanamu, ambazo sanamu zao za kuchongwa zilikuwa bora kuliko sanamu za Yerusalemu na za Samaria;
11. je! Sitautenda Yerusalemu na sanamu zake vile vile kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake?
12. Basi, itakuwa, Bwana atakapokuwa ameitimiza kazi yake yote juu ya mlima Sayuni na juu ya Yerusalemu, nitayaadhibu matunda ya kiburi cha moyo wake mfalme wa Ashuru, na majivuno ya macho yake.