Hes. 9:13-22 Swahili Union Version (SUV)

13. Lakini mtu aliye safi, wala hakuwa katika safari, naye amekosa kuishika Pasaka, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake; kwa sababu hakumtolea BWANA matoleo kwa wakati wake ulioamriwa, mtu huyo atachukua dhambi yake.

14. Na kama mgeni akiketi kati yenu ugenini, naye ataka kuishika Pasaka kwa BWANA; kama hiyo sheria ya Pasaka ilivyo, na kama amri yake ilivyo, ndivyo atakavyofanya; mtakuwa na sheria moja, kwa huyo aliye mgeni, na kwa huyo aliyezaliwa katika nchi.

15. Na siku hiyo maskani iliposimamishwa, lile wingu likaifunika maskani, yaani, hema ya kukutania; wakati wa jioni likawa juu ya maskani, mfano wa moto, hata asubuhi.

16. Ndivyo ilivyokuwa sikuzote; lile wingu liliifunika kwa mfano wa moto usiku.

17. Na kila lilipoinuliwa lile wingu juu ya ile Hema ndipo wana wa Israeli waliposafiri; na mahali lilipokaa lile wingu, ndipo wana wa Israeli walipopiga kambi yao.

18. Kwa amri ya BWANA Wana wa Israeli walisafiri, na kwa amri ya BWANA walipiga kambi; wakati lile wingu ilipokaa juu ya maskani walikaa katika kambi yao.

19. Na lile wingu lilipokawia juu ya maskani siku nyingi, ndipo wana wa Israeli walipolinda malinzi ya BWANA, wala hawakusafiri.

20. Na pengine lile wingu lilikaa juu ya maskani siku chache; ndipo kwa amri ya BWANA walikaa katika kambi yao, tena kwa amri ya BWANA walisafiri.

21. Na pengine lile wingu lilikaa tangu jioni hata asubuhi; na lile wingu lilipoinuliwa asubuhi walisafiri, au kama likikaa usiku na mchana pia, lilipoinuliwa lile wingu, ndipo waliposafiri.

22. Ikiwa lile wingu lilikawia, likikaa juu ya maskani siku mbili, au mwezi, au mwaka, wana wa Israeli walikaa katika kambi yao, wasisafiri;

Hes. 9