5. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
6. Uwaambie wana wa Israeli, Mtu mume au mke atakapofanya dhambi yo yote, ifanywayo na binadamu, kumwasi BWANA, na mtu huyo akawa na hatia;
7. ndipo watakapoungama dhambi yao waliyoifanya; naye atarudisha kwa hatia yake, kwa utimilifu wake, tena ataongeza juu yake sehemu ya tano, na kumpa huyo aliyemkosa.
8. Lakini kwamba mtu huyo hana jamaa ya karibu ambaye inampasa kurudishiwa kwa ajili ya hiyo hatia, kile kitakachorudishwa kwa BWANA kwa hiyo hatia kitakuwa cha kuhani, pamoja na kondoo mume wa upatanisho, ambaye kwa huyo utafanywa upatanisho kwa ajili yake.
9. Tena kila sadaka ya kuinuliwa, ya vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, watakavyosongeza kwa kuhani, itakuwa ni yake.
10. Tena vitu vilivyowekwa wakfu na mtu awaye yote, vitakuwa ni vya kuhani; kitu cho chote mtu atakachompa kuhani, kitakuwa chake.
11. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
12. Nena na wana wa israeli, uwaambie, kama mke wa mtu ye yote akikengeuka, na kumkosa mumewe,
13. na mtu mume akalala naye kwa uasherati, na jambo hilo likamfichamania mumewe, likawa jambo lisilojulikana, na huyo mwanamke akawa najisi, wala hapana shahidi aliyeshuhudia juu yake, wala hakufumaniwa;
14. kisha mumewe akashikwa na roho ya wivu, akamwonea wivu mkewe, naye akawa najisi huyo mwanamke; au kama akiingiwa na roho ya wivu, akamwonea wivu mkewe, naye hakuwa na unajisi huyo mke;
15. ndipo huyo mume atamchukua mkewe, aende naye kwa kuhani, naye ataleta sadaka yake kwa ajili yake, yaani, sehemu ya kumi ya efa ya unga wa shayiri; asitie mafuta juu yake, wala asitie ubani juu yake; maana, ni sadaka ya unga ya wivu, ni sadaka ya unga ya ukumbusho ya kukumbukia uovu.
16. Basi kuhani atamleta mwanamke akaribie, na kumweka mbele za BWANA;
17. kisha kuhani atatwaa maji matakatifu katika chombo cha udongo; kisha kuhani atatwaa katika vumbi lililo pale chini ya maskani, na kulitia katika hayo maji;