Hes. 4:22-40 Swahili Union Version (SUV)

22. Fanya jumla ya wana wa Gershoni nao, kwa nyumba za baba zao, na jamaa zao;

23. tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini utawahesabu; wote watakaoingia kutumika, ili kufanya kazi katika hema ya kukutania.

24. Huu ni utumishi wa jamaa za Wagershoni, katika kutumika na katika kuchukua mizigo;

25. wao watayachukua mapazia ya maskani, na hema ya kukutania, hizo nguo za kufunikia, na zile ngozi za pomboo za kufunikia zilizo juu yake, na pazia la mlango wa hema ya kukutania;

26. na kuta za nguo za ua, na sitara ya ile nafasi ya kuingilia ya lango la ua, ulio karibu na maskani na madhabahu, kuzunguka pande zote, na kamba zake, na vyombo vyote vya utumishi wao, na yote yatakayotendeka kwavyo, watatumika katika hayo.

27. Utumishi wote wa wana wa Wagershoni, katika mzigo wao wote, na utumishi wao wote, utakuwa kwa amri ya Haruni na wanawe; nanyi mtawaagizia mzigo wao wote kuulinda.

28. Huu ni utumishi wa jamaa za wana wa Wagershoni katika hema kukutania; na ulinzi utakuwa chini ya mkono wa Ithamari mwana wa Haruni kuhani.

29. Katika habari ya wana wa Merari, utawahesabu kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao;

30. tangu aliyepata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, utawahesabu, kila atakayeingia katika huo utumishi, ili kufanya kazi ya hema ya kukutania.

31. Na mausia ya mzigo wao ni haya, kwa utumishi wao wote katika hema ya kukutania; mbao za maskani, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake;

32. na viguzo vya ua vya kuuzunguka pande zote, na matako yake, na vigingi vyake, na kamba zake, na vyombo vyake vyote, pamoja na utumishi wake wote; nanyi mtawaagizia kila mtu kwa jina lake vile vyombo vya mzigo wao watakaoulinda.

33. Huu ni utumishi wa jamaa za wana wa Merari, kwa utumishi wao wote, katika hema ya kukutania, chini ya mkono wa Ithamari mwana wa Haruni kuhani.

34. Basi Musa na Haruni na hao wakuu wa mkutano wakawahesabu wana wa Kohathi kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao,

35. tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, kila mtu aliyeingia katika utumishi kwa kazi katika hema ya kukutania,

36. na waliohesabiwa kwao kwa jamaa zao, walikuwa elfu mbili na mia saba hamsini.

37. Hao ndio waliohesabiwa katika jamaa za Wakohathi, wote waliotumika katika hema ya kukutania, ambao Musa na Haruni waliwahesabu kwa amri ya BWANA kwa mkono wa Musa.

38. Na hao waliohesabiwa katika wana wa Gershoni, kwa jamaa zao na nyumba zao baba zao,

39. tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, kila mtu aliyeingia katika utumishi, kwa kazi katika hema ya kukutania,

40. hata wale waliohesabiwa kwao, kwa jamaa zao na nyumba za baba zao, walikuwa elfu mbili na mia sita na thelathini.

Hes. 4