3. Hiyo miji watakuwa nayo ili wakae humo, na malisho watakuwa nayo kwa wanyama wao wa mifugo, na kwa mali zao, na kwa wanyama wao wote.
4. Na yale malisho ya miji mtakayowapa Walawi, ukubwa wake utakuwa tangu ukuta wa mji kupima kiasi cha dhiraa elfu pande zote.
5. Nanyi mtapima hapo nje ya mji upande wa mashariki dhiraa elfu mbili, na upande wa kusini dhiraa elfu mbili, na upande wa magharibi dhiraa elfu mbili, na upande wa kaskazini dhiraa elfu mbili, huo mji ulio katikati. Hayo ndiyo yatakayokuwa kwao malisho ya miji.
6. Na hiyo miji mtakayowapa Walawi, itakuwa miji sita ya makimbilio, mtakayoweka kwa ajili ya mwenye kumwua mtu, ili akimbilie huko; pamoja na hiyo mtawapa miji arobaini na miwili zaidi.
7. Miji yote mtakayowapa hao Walawi jumla yake itakuwa miji arobaini na minane; mtawapa miji hiyo pamoja na malisho yake.
8. Tena katika miji mtakayotoa ya hiyo milki ya wana wa Israeli, katika hao walio wengi mtatwaa miji mingi; na katika hao walio wachache mtatwaa miji michache; kila mtu kama ulivyo urithi wake atakaourithi, atawapa Walawi katika miji yake.
9. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
10. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani,
11. Ndipo mtajiwekea miji iwe miji ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.
12. Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe.
13. Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa kwenu ni miji sita ya makimbilio.
14. Mtawapa miji mitatu ng’ambo ya pili ya Yordani, na miji mitatu mtawapa katika nchi ya Kanaani; miji hiyo itakuwa ni miji ya makimbilio.
15. Miji hiyo sita itakuwa miji ya makimbilio kwa ajili ya wana wa Israeli, na kwa ajili ya mgeni, na kwa ajili ya huyo aketiye kati yao hali ya ugeni; ili kila amwuaye mtu, naye hakukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.
16. Lakini kama alimpiga kwa chombo cha chuma, akafa, ni mwuaji huyo; mwuaji hakika yake atauawa.
17. Na kama alimpiga kwa jiwe lililokuwa mkononi mwake, ambalo kwa hilo humkini mtu kufa, naye akafa, yeye ni mwuaji; huyo mwuaji lazima atauawa.
18. Au kama alimpiga kwa chombo cha mti kilichokuwa mkononi mwake ambacho kwa hicho humkini mtu kufa, naye akafa, ni mwuaji huyo, mwuaji lazima atauawa.
19. Mwenye kutwaa kisasi cha damu ndiye atakayemwua mwuaji; hapo atakapokutana naye, atamwua.
20. Tena kwamba alimsukuma kwa kumchukia, au kwamba alimtupia kitu kwa kumvizia, hata akafa;