10. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani,
11. Ndipo mtajiwekea miji iwe miji ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.
12. Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe.
13. Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa kwenu ni miji sita ya makimbilio.
14. Mtawapa miji mitatu ng’ambo ya pili ya Yordani, na miji mitatu mtawapa katika nchi ya Kanaani; miji hiyo itakuwa ni miji ya makimbilio.
15. Miji hiyo sita itakuwa miji ya makimbilio kwa ajili ya wana wa Israeli, na kwa ajili ya mgeni, na kwa ajili ya huyo aketiye kati yao hali ya ugeni; ili kila amwuaye mtu, naye hakukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.
16. Lakini kama alimpiga kwa chombo cha chuma, akafa, ni mwuaji huyo; mwuaji hakika yake atauawa.
17. Na kama alimpiga kwa jiwe lililokuwa mkononi mwake, ambalo kwa hilo humkini mtu kufa, naye akafa, yeye ni mwuaji; huyo mwuaji lazima atauawa.
18. Au kama alimpiga kwa chombo cha mti kilichokuwa mkononi mwake ambacho kwa hicho humkini mtu kufa, naye akafa, ni mwuaji huyo, mwuaji lazima atauawa.
19. Mwenye kutwaa kisasi cha damu ndiye atakayemwua mwuaji; hapo atakapokutana naye, atamwua.
20. Tena kwamba alimsukuma kwa kumchukia, au kwamba alimtupia kitu kwa kumvizia, hata akafa;
21. au akampiga kwa mkono wake kwa kuwa ni adui, naye akafa; yeye aliyempiga lazima atauawa; yeye ni mwuaji; mwenye kutwaa kisasi cha damu atamwua mwuaji, hapo atakapokutana naye.
22. Lakini ikiwa alimsukuma ghafula pasipo kumchukia; au akamtupia kitu cho chote pasipo kumvizia,
23. au kwa jiwe liwalo lote, ambalo kwa kupigwa kwalo humkini mtu kufa, asipomwona, akamtupia hata akafa, naye hakuwa adui yake, wala hakumtakia madhara;
24. ndipo mkutano utaamua kati ya huyo aliyempiga mtu na huyo atakayetwaa kisasi cha damu, kama hukumu hizi zilivyo;
25. nao mkutano utamwokoa yule aliyemwua mtu na mkono wa mwenye kutwaa kisasi cha damu; tena mkutano utamrejeza katika mji wake wa makimbilio, aliokuwa anaukimbilia; naye atakaa humo hata kifo chake kuhani mkuu, aliyepakwa mafuta kwa mafuta matakatifu.
26. Lakini kama mwenye kumwua mtu akienda wakati wo wote kupita mpaka wa huo mji wa makimbilio, alioukimbilia;
27. na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwona, naye yu nje ya mpaka wa mji wake wa makimbilio, na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwua huyo mwuaji, hatakuwa na hatia ya damu;