Hes. 3:20-38 Swahili Union Version (SUV)

20. Na wana wa Merari kwa jamaa zao ni Mahli, na Mushi. Hizi ndizo jamaa za Walawi kwa nyumba za baba zao.

21. Katika Gershoni walikuwa jamaa ya Walibni, na jamaa ya Washimei, hawa ndio jamaa za Wagershoni.

22. Hao waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, hao waliohesabiwa kwao walikuwa saba elfu na mia tano.

23. Jamaa za Wagershoni watapanga rago nyuma ya maskani, upande wa magharibi.

24. Na mkuu wa nyumba ya baba zao Wagershoni atakuwa Eliasafu mwana wa Laeli.

25. Na ulinzi wa Wagershoni katika hema ya kukutania ni hiyo maskani, na Hema, na kifuniko chake, na pazia la mlango wa hema ya kukutania,

26. na kuta za nguo za ua, na sitara ya mlango wa ua, iliyo karibu na maskani, na karibu na madhabahu pande zote, na kamba zake zitumiwazo kwa matumizi yake yote.

27. Na katika Kohathi ni jamaa ya Waamrami, na jamaa ya Waishari, na jamaa ya Wahebroni, na jamaa ya hao Wauzieli; hizo ni jamaa za Wakohathi.

28. Kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa elfu nane na mia sita, wenye kuulinda ulinzi wa mahali patakatifu.

29. Jamaa za wana wa Kohathi watapanga rago upande wa kusini wa maskani.

30. Na mkuu wa nyumba ya baba za jamaa za Wakohathi atakuwa Elisafani mwana wa Uzieli.

31. Na vitu watakavyovitunza ni hilo sanduku, na meza, na kinara cha taa, na madhabahu, na vile vyombo vya mahali patakatifu wavitumiavyo katika kutumika kwao, na pazia, na utumishi wake wote.

32. Na Eleazari mwana wa Haruni kuhani atakuwa mkuu wa hao wakuu wa Walawi, naye atawasimamia hao walindao ulinzi wa mahali patakatifu.

33. Katika Merari ni jamaa ya hao Wamahli, na jamaa ya Wamushi; hizo ni jamaa za Merari.

34. Na hao waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa sita elfu na mia mbili.

35. Na mkuu wa nyumba ya baba za jamaa za Merari alikuwa Surieli mwana wa Abihaili; hao watapanga rago upande wa maskani, wa kaskazini.

36. Na usimamizi walioamriwa wana wa Merari ulikuwa ni kutunza mbao za maskani, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake, na vyombo vyake vyote, na utumishi wake wote;

37. na nguzo za ua zilizouzunguka, na matako yake, na vigingi vyake, na kamba zake.

38. Na hao watakaopanga mbele ya maskani upande wa mashariki, mbele ya hema ya kukutania upande wa kuelekea maawio ya jua, watakuwa hawa, Musa na Haruni na wanawe, wenye kulinda ulinzi wa mahali patakatifu, yaani, huo ulinzi wa wana wa Israeli; na mgeni atakayekaribia atauawa.

Hes. 3