Hes. 18:8-19 Swahili Union Version (SUV)

8. Kisha BWANA akamwambia Haruni, Tazama, nimekupa wewe ulinzi wa sadaka zangu za kuinuliwa, maana, vitu vyote vya hao wana wa Israeli vilivyowekwa wakfu; nimekupa wewe na wanao vitu hivyo kwa ajili ya kule kutiwa mafuta kwenu, kuwa haki yenu milele.

9. Vitu hivi vitakuwa vyako katika vile vilivyo vitakatifu sana, visiteketezwe motoni; matoleo yao yote, maana, kila sadaka yao ya unga, na kila sadaka yao ya dhambi, na kila sadaka yao ya hatia watakayonitolea, vitakuwa vitakatifu sana kwa ajili yako wewe na kwa wanao.

10. Utakula vitu hivyo kuwa ni vitu vitakatifu sana; kila mume atakula vitu hivyo; vitakuwa vitakatifu kwako wewe.

11. Tena kitu hiki ni chako; ile sadaka ya kuinuliwa ya kipawa chao, maana, sadaka za kutikiswa zote za wana wa Israeli; hizi nimekupa wewe, na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu milele; kila mtu katika nyumba yako aliye safi atakula katika hizo.

12. Yaliyo mazuri katika mafuta, na yaliyo mazuri ya mavuno ya zabibu, na ya mavuno ya nafaka, malimbuko yake watakayompa BWANA, amekupa wewe hayo.

13. Matunda ya kwanza yaivayo katika yote yaliyo katika nchi yao, watakayomletea BWANA, yatakuwa yako, kila mtu aliye safi katika nyumba yako atakula katika vitu hivyo.

14. Kila kitu kilichowekwa wakfu katika Israeli kitakuwa chako.

15. Kila kifunguacho tumbo, cha wenye mwili wote watakachomsongezea BWANA cha wanadamu na cha wanyama, ni chako; lakini mzaliwa wa kwanza wa binadamu, huna budi utamkomboa, na mzaliwa wa kwanza wa wanyama wasio safi utamkomboa.

16. Na hao watakaokombolewa katika wanyama hao, tangu aliyepata umri wa mwezi mmoja utamkomboa, kama utakavyohesabu kima chake, kwa fedha ya shekeli tano, kwa shekeli ya mahali patakatifu (nayo ni gera ishirini).

17. Lakini mzaliwa wa kwanza wa ng’ombe, au mzaliwa wa kwanza wa kondoo, au mzaliwa wa kwanza wa mbuzi, hutawakomboa hao; maana, ni watakatifu hao; utanyunyiza damu yao katika madhabahu, na kuyateketeza mafuta yao kuwa sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto, iwe harufu ya kupendeza.

18. Tena nyama yao itakuwa ni yako wewe, kama kile kidari cha kutikiswa, na kama mguu wa nyuma wa upande wa kuume, itakuwa yako.

19. Sadaka zote za kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa BWANA, nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni agano la chumvi la milele mbele za BWANA kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja nawe.

Hes. 18