Hes. 15:2-16 Swahili Union Version (SUV)

2. Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Mtakapoingia nchi yenu ya kukaa, niwapayo,

3. nanyi mwataka kumsongezea BWANA sadaka kwa moto, kwamba ni sadaka ya kuteketezwa, au dhabihu ya kuchinjwa, ili kuondoa nadhiri, au kuwa sadaka ya hiari, au katika sikukuu zenu zilizoamriwa, ili kumfanyia BWANA harufu ipendezayo, katika ng’ombe, au katika kondoo;

4. ndipo yeye atakayetoa matoleo yake na amtolee BWANA sadaka ya unga ya sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta;

5. na divai kwa sadaka ya kinywaji, robo ya hini, utaiandaa pamoja na sadaka ya kuteketezwa, au kwa dhabihu ya kuchinjwa, kwa ajili ya kila mwana-kondoo.

6. Au kwa ajili ya kondoo mume, utaiandaa sadaka ya unga ya sehemu za kumi mbili za efa ya unga mwembamba uliochanganywa na sehemu ya tatu ya hini ya mafuta;

7. na kwa sadaka ya kinywaji utasongeza sehemu ya tatu ya hini ya divai, kuwa harufu ya kupendeza kwa BWANA.

8. Tena hapo utakapomwandaa ng’ombe mume kwa sadaka ya kuteketezwa, au kwa dhabihu ya kuchinjwa, kwa kuondoa nadhiri, au kwa sadaka za amani kwa BWANA;

9. ndipo utakapotoa, pamoja na huyo ng’ombe, sadaka ya unga ya sehemu za kumi tatu za efa ya unga mwembamba uliochanganywa na nusu ya hini ya mafuta.

10. Tena utasongeza nusu ya hini ya divai kwa sadaka ya kinywaji, kwa sadaka iliyosongezwa kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA.

11. Ndivyo itakavyofanywa kwa kila ng’ombe, au kwa kila kondoo mume, au kwa kila mwana-kondoo mume, au kila mwana-mbuzi.

12. Kama hesabu ilivyo ya hao mtakaowaandaa, ndivyo mtakavyofanya kwa kila mmoja, sawasawa na hesabu yao.

13. Wote ambao wamezaliwa kwenu watafanya hayo yote kwa kuandama mfano huo, katika kusongeza sadaka kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA.

14. Tena kwamba mgeni amekaa kwenu, au mtu ye yote aliye kati yenu katika vizazi vyenu, naye yuataka kusongeza sadaka kwa moto, na harufu ya kupendeza kwa BWANA; kama ninyi mfanyavyo, na yeye atafanya vivyo.

15. Katika huo mkutano, kutakuwa na amri moja kwenu ninyi na kwa mgeni akaaye pamoja nanyi; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; kama ninyi mlivyo, na mgeni atakuwa vivyo mbele za BWANA.

16. Itakuwa sheria moja na amri moja kwenu ninyi na kwa mgeni akaaye nanyi.

Hes. 15