1. Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule.
2. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.
3. Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?
4. Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri.
5. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli.
6. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao;
7. wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu.
8. Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali.
9. Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope.
10. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.