1. Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu.
2. BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.
3. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.
4. Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.
5. Naam, pamoja na hayo, divai ni mchumi mdanganyifu, mtu wa kiburi asiyekaa nyumbani mwake; huongeza tamaa yake kama kuzimu, naye huwa kama mauti, hawezi kushibishwa; bali hujikusanyia mataifa yote; hujiwekea kabila zote chungu chungu.
6. Je! Hawa wote hawatapiga mfano juu yake, na mithali ya kusimanga juu yake, wakisema, Ole wake yeye aongezaye kisicho mali yake! Hata lini? Na ole wake yeye ajitwikaye mzigo wa rehani!
7. Je! Hawatainuka ghafula wao watakaokuuma, hawataamka wao watakaokusumbua, nawe utakuwa mateka kwao?
8. Kwa sababu umeteka nyara mataifa mengi, mabaki yote ya kabila watakuteka wewe; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake.
9. Ole wake yeye aipatiaye nyumba yake mapato mabaya, ili apate kukiweka kioto chake juu, apate kujiepusha na mkono wa uovu!
10. Wewe umeifanyia nyumba yako kusudi la aibu, kwa kukatilia mbali watu wengi, nawe umetenda dhambi juu ya roho yako.