25. nami nikawapimia kwa mizani zile fedha, na dhahabu, na vile vyombo, matoleo kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu, ambayo mfalme, na washauri wake, na wakuu wake, na Israeli wote waliokuwapo, walikuwa wameyatoa;
26. nami nikawapimia mikononi mwao talanta za fedha mia sita na hamsini na vyombo vya fedha talanta mia; na talanta mia za dhahabu;
27. na mabakuli ishirini ya dhahabu, thamani yake darkoni elfu; na vyombo viwili vya shaba nzuri iliyong’aa, thamani yake sawa na dhahabu.
28. Kisha nikawaambia, Ninyi mmekuwa watakatifu kwa BWANA, na hivyo vyombo ni vitakatifu; na fedha na dhahabu ni matoleo ya hiari kwa BWANA, Mungu wa baba zenu.
29. Basi, angalieni, na kuvitunza vitu hivi, hata mtakapovipima mbele ya wakuu wa makuhani, na Walawi, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli, huko Yerusalemu, katika vyumba vya nyumba ya BWANA.
30. Hivyo makuhani na Walawi wakaupokea uzani wa fedha, na dhahabu, na vyombo, ili kuvileta Yerusalemu nyumbani kwa Mungu wetu.
31. Ndipo tukasafiri toka mtoni Ahava siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza, ili kwenda Yerusalemu; na mkono wa Mungu ulikuwa pamoja nasi, akatuokoa na mkono wa adui, na mtu mwenye kutuvizia njiani.
32. Tukafika Yerusalemu, tukakaa huko muda wa siku tatu.
33. Hata siku ya nne, hizo fedha na dhahabu na vile vyombo vilipimwa ndani ya nyumba ya Mungu, vikatiwa mikononi mwa Meremothi, mwana wa Uria, kuhani; na pamoja naye alikuwapo Eleazari, mwana wa Finehasi; na pamoja nao Yozabadi, mwana wa Yeshua, na Noadia, mwana wa Binui, Walawi;