17. Nikawapeleka kwa Ido, mkuu, huko Kasifia; nikawaambia watakayomwambia Ido, na ndugu zake hao Wanethini, huko Kasifia, kwamba watuletee watu watakaohudumu katika nyumba ya Mungu wetu.
18. Na kama mkono mwema wa Mungu wetu ulivyokuwa pamoja nasi, wakamletea Ishekeli, mmoja wa wana wa Mali, mwana wa Lawi, mwana wa Israeli; na Sherebia, pamoja na wanawe na ndugu zake, watu kumi na wanane;
19. na Hashabia, na pamoja naye Yeshaya, wa wana wa Merari, na ndugu zake na wana wao, watu ishirini;
20. na katika Wanethini, ambao Daudi, na wakuu, walikuwa wamewaweka kwa ajili ya utumishi wa Walawi, Wanethini mia mbili na ishirini; wote wametajwa kwa majina yao.
21. Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za Mungu, na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote.
22. Maana naliona haya kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapanda farasi, ili kutusaidia juu ya adui njiani; kwa maana tulikuwa tumesema na mfalme, tukinena, Mkono wa Mungu u juu ya watu wote wamtafutao, kuwatendea mema; bali uweza wake na ghadhabu yake ni kinyume cha wote wamwachao.
23. Basi tukafunga, tukamsihi Mungu wetu kwa ajili ya hayo; naye akatutakabali.
24. Ndipo nikawatenga watu kumi na wawili wa wakuu wa makuhani, nao ni Sherebia, na Hashabia, na watu kumi wa ndugu zao pamoja nao,
25. nami nikawapimia kwa mizani zile fedha, na dhahabu, na vile vyombo, matoleo kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu, ambayo mfalme, na washauri wake, na wakuu wake, na Israeli wote waliokuwapo, walikuwa wameyatoa;