Ezr. 7:14-25 Swahili Union Version (SUV)

14. Kwa kuwa umetumwa na mfalme, na washauri wake saba, ili kuuliza habari za Yuda na Yerusalemu, kwa sheria ya Mungu wako iliyo mkononi mwako;

15. na kuichukua fedha na dhahabu, ambayo mfalme, na washauri wake, kwa hiari yao, wamemtolea Mungu wa Israeli, akaaye Yerusalemu;

16. na fedha yote na dhahabu utakayoona katika wilaya ya Babeli, pamoja na vitu watakavyotoa watu kwa hiari yao, na vitu vya makuhani walivyotoa kwa hiari yao, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu.

17. Kwa sababu hiyo ujitahidi kununua kwa fedha hiyo mafahali, kondoo waume, wana-kondoo, pamoja na sadaka zao za unga, na sadaka zao za kinywaji; nawe utazitoa juu ya madhabahu ya nyumba ya Mungu wenu, iliyoko Yerusalemu.

18. Na neno lo lote mtakaloona vema kulitenda, wewe na ndugu zako, kwa ile fedha na dhahabu itakayobaki, hilo litendeni, kama apendavyo Mungu wenu.

19. Na vile vyombo upewavyo kwa huduma ya nyumba ya Mungu wako, virejeze mbele za Mungu wa Yerusalemu.

20. Na cho chote kitakachohitajiwa zaidi, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wako, kitakachokupasa kukitoa, kitoe katika nyumba ya hazina ya mfalme.

21. Na mimi, naam mimi, mfalme Artashasta, nawapa amri wote wenye kutunza hazina, walio ng’ambo ya Mto, ya kwamba, kila neno ambalo Ezra, kuhani, mwandishi wa torati ya Mungu wa mbinguni, atalitaka kwenu, na litendeke kwa bidii nyingi,

22. hata kiasi cha talanta mia za fedha, na vipimo mia vya ngano, na bathi mia za divai, na bathi mia za mafuta, na chumvi bila kuuliza kiasi chake.

23. Kila neno litakaloamriwa na Mungu wa mbinguni, na litendeke halisi kwa ajili ya nyumba ya Mungu wa mbinguni. Kwa nini itokee ghadhabu juu ya ufalme wa mfalme na wanawe?

24. Tena twawaarifuni ya kuwa katika habari ya makuhani, na Walawi, na waimbaji, na mabawabu na Wanethini, au watumishi wa nyumba hii ya Mungu, si halali kuwatoza kodi, wala ada, wala ushuru.

25. Na wewe, Ezra, kwa kadiri ya hekima ya Mungu wako iliyo mkononi mwako, waweke waamuzi na makadhi, watakaowahukumu watu wote walio ng’ambo ya Mto, yaani, wote wenye kuzijua amri za Mungu wako; ukamfundishe yeye asiyezijua.

Ezr. 7