Ezr. 6:10-21 Swahili Union Version (SUV)

10. wapate kumtolea Mungu wa mbinguni sadaka zenye harufu nzuri, na kumwombea mfalme, na wanawe, wapate uzima.

11. Pia nimetoa amri kwamba, mtu awaye yote atakayelibadili neno hili, boriti na itolewe katika nyumba yake, akainuliwe na kutungikwa juu yake; tena nyumba yake ikafanywe jaa kwa ajili ya neno hili.

12. Na Mungu huyu, aliyelifanya jina lake likae pale, na aangamize wafalme wote, na watu wote, watakaonyosha mikono yao kulibadili neno hili, na kuiharibu nyumba hii ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Mimi, Dario, nimetoa amri; na ifanyike kwa bidii nyingi.

13. Ndipo Tatenai, liwali wa ng’ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzi wao, wakafanya hayo kwa bidii, kwa sababu mfalme Dario alikuwa ametuma watu kwao.

14. Nao wazee wa Wayahudi wakajenga, wakafanikiwa, kwa msaada wa kuhubiri kwao Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido. Wakajenga, wakaimaliza kazi yao, kwa maagizo ya Mungu wa Israeli, na kwa amri ya Koreshi, na Dario, na Artashasta mfalme wa Uajemi.

15. Nyumba hiyo ikamalizika siku ya tatu ya mwezi Adari, katika mwaka wa sita wa kutawala kwake mfalme Dario.

16. Na wana wa Israeli, na makuhani na Walawi, na watu wengine katika hao waliohamishwa, wakaiweka wakfu nyumba ya Mungu kwa furaha.

17. Na katika kuiweka wakfu nyumba ya Mungu, wakatoa sadaka, ng’ombe mia, na kondoo waume mia mbili, na wana-kondoo mia nne; tena wakatoa mbuzi waume kumi na wawili, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli wote, kwa hesabu ya kabila za Israeli.

18. Wakawaweka makuhani katika kura zao, wakawaweka na Walawi katika zamu zao, kwa ajili ya huduma ya Mungu, iliyokuwako Yerusalemu; vile vile kama vilivyoandikwa katika chuo cha Musa.

19. Kisha, wana wa uhamisho wakaifanya Pasaka, mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne ya mwezi.

20. Kwa maana makuhani na Walawi walikuwa wamejitakasa wote pamoja; wote walikuwa hali ya tohara; wakachinja Pasaka kwa ajili ya wana wote wa uhamisho, na kwa ajili ya ndugu zao makuhani, na kwa ajili ya nafsi zao.

21. Wana wa Israeli wakaila, wale waliorudi kuitoka nchi ya uhamisho wao, na watu wote ambao pamoja nao wamejitenga na uchafu wa taifa za nchi, ili kumtaka BWANA, Mungu wa Israeli,

Ezr. 6