Ezr. 4:3-10 Swahili Union Version (SUV)

3. Lakini Zerubabeli, na Yoshua, na wakuu wengine wa mbari za mababa katika Israeli, wakawaambia, Ninyi haiwahusu kushirikiana nasi katika kumjengea Mungu wetu nyumba; bali sisi wenyewe peke yetu tutamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba, kama mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi, alivyotuamuru.

4. Ndipo watu wa nchi wakaidhoofisha mikono ya watu wa Yuda, wakawasumbua, walipokuwa wakijenga.

5. Wakawaajiri washauri juu yao, ili kuwapinga kusudi lao, siku zote za Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata wakati wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi.

6. Tena, wakati wa kutawala kwake Ahasuero, mwanzo wa kutawala kwake, watu wakaandika mashitaka juu ya wenyeji wa Yuda na Yerusalemu.

7. Na tena, katika siku za Artashasta, Mithredathi, na Tabeeli na mabaki ya wenziwe, wakimwandikia Artashasta, mfalme wa Uajemi, salamu za heri; na mwandiko wa waraka huo, ukaandikwa kwa herufi za Kiaramu, na kunenwa kwa lugha ya Kiaramu.

8. Nao Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, wakaandika waraka juu ya Yerusalemu kwa Artashasta, mfalme, kama hivi;

9. Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, na mabaki ya wenzao, makadhi wa Kiajemi na madiwani wa Kiajemi; na Waarkewi, Wababeli, Washushani, yaani, Waelami;

10. na mabaki ya mataifa, ambao Asur-bani-pali mkuu, mwenye heshima, aliwavusha, na kuwakalisha katika mji wa Samaria, na mahali penginepo, ng’ambo ya Mto; wakadhalika.

Ezr. 4