1. Basi hapo Ezra alipokuwa akiomba na kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, wakamkusanyikia katika Israeli wote kusanyiko kubwa sana la wanaume, na wanawake, na watoto; maana watu hao walikuwa wakilia sana.
2. Hata Shekania, mwana wa Yehieli, mmoja wa wana wa Elamu, akajibu, akamwambia Ezra, Sisi tumemkosa Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi; lakini kungaliko tumaini kwa Israeli katika jambo hili.
3. Haya basi! Na tufanye agano na Mungu wetu, kuachana na wake zetu, na wale waliozaliwa nao, tukilifuata shauri la bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya na yatendeke kwa kuifuata torati.
4. Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende.
5. Ndipo Ezra akaondoka, akawaapisha wakuu wa makuhani, na Walawi, na Israeli wote, ya kwamba watafanya kama hayo. Basi wakaapa.
6. Kisha Ezra akaondoka hapo mbele ya nyumba ya Mungu, akaingia katika chumba cha Yehohanani, mwana wa Eliashibu; hata, alipofika huko, hakula mkate, wala hakunywa maji; kwa maana alilia kwa sababu ya kosa lile la watu wa uhamisho.
7. Wakapiga mbiu katika Yuda yote na Yerusalemu, ya kwamba wana wote wa uhamisho wakusanyike pamoja huko Yerusalemu;
8. na ya kwamba mtu awaye yote asiyekuja katika muda wa siku tatu, kwa shauri lile la wakuu na wazee, basi aondolewe mali zake zote, akatengwe yeye mwenyewe na mkutano wa uhamisho.