Eze. 8:10-18 Swahili Union Version (SUV)

10. Basi, nikaingia, nikaona; na tazama, kila namna ya wadudu, na wanyama wachukizao, na taswira za vinyago vyote vya nyumba ya Israeli, zimepigwa ukutani pande zote.

11. Na watu sabini wa wazee wa Israeli walikuwa wamesimama na kuzielekea, na katikati yao alisimama Yaazania, mwana wa Shafani; kila mmoja ana chetezo mkononi mwake, na harufu ya moshi wa uvumba ilipaa juu.

12. Kisha akaniambia, Mwanadamu, umeyaona wanayotenda wazee wa nyumba ya Israeli gizani, kila mtu ndani ya vyumba vyake vya sanamu? Maana husema, BWANA hatuoni; BWANA ameiacha nchi hii.

13. Akaniambia tena, Utaona tena machukizo makubwa mengine wanayoyatenda.

14. Ndipo akanileta mpaka mlango wa kuingilia katika nyumba ya BWANA, ulioelekea upande wa kaskazini, na tazama, wanawake wameketi wakimlilia Tamuzi.

15. Akaniambia, Mwanadamu umeyaona haya? Utaona tena machukizo makubwa kuliko hayo.

16. Akanileta mpaka ua wa ndani wa nyumba ya BWANA, na tazama, mlangoni pa hekalu la BWANA, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwako watu kama ishirini na watano, wamelipa kisogo hekalu la BWANA, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki, nao wanaliabudu jua, kwa kuuelekea upande wa mashariki.

17. Basi, akaniambia, Umeyaona haya, Ee mwanadamu? Je! Ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda, wayafanye machukizo wanayoyafanya hapa? Kwa maana wameijaza nchi hii udhalimu, tena wamerejea nyuma ili kunikasirisha; na, tazama, wanaliweka tawi puani.

18. Kwa sababu hiyo mimi nami nitatenda kwa ghadhabu; jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma, na wajapolia masikioni mwangu kwa sauti kuu, sitawasikiliza.

Eze. 8