8. Lakini nitasaza mabaki; maana mtakuwa na baadhi ya watu watakaoukimbia upanga kati ya mataifa, mtakapokuwa mmetawanyika katika nchi za watu.
9. Na hao wa kwenu watakaookoka watanikumbuka kati ya mataifa, watakakochukuliwa mateka, jinsi nilivyoiponda mioyo yao ya kikahaba, iliyoniacha, na macho yao, yaendayo kufanya uasherati na vinyago vyao; nao watajichukia nafsi zao machoni pao wenyewe, kwa sababu ya mabaya yao yote, waliyoyatenda kwa machukizo yao yote.
10. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; sikusema bure kama nitawatenda mabaya hayo.
11. Bwana MUNGU asema hivi; Piga kwa mkono wako, ipige nchi kwa mguu wako, ukaseme, Ole! Kwa sababu ya machukizo maovu yote ya nyumba ya Israeli; maana wataanguka kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni.
12. Yeye aliye mbali sana atakufa kwa tauni; na yeye aliye karibu atakufa kwa upanga; na yeye atakayesalia, na kuhusuriwa katika mji, atakufa kwa njaa, hivyo ndivyo nitakavyoitimiza ghadhabu yangu juu yao.