Eze. 5:11-17 Swahili Union Version (SUV)

11. Kwa sababu hiyo, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa kuwa umepatia unajisi patakatifu pangu, kwa matendo yako yote niyachukiayo, na kwa machukizo yako yote, kwa sababu hiyo mimi nami nitakupunguza; wala jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma.

12. Theluthi yenu mtakufa kwa tauni, na kwa njaa watakomeshwa ndani yako; na theluthi yenu wataanguka kwa upanga pande zako zote; na theluthi yenu nitawatawanya kwa pepo zote, kisha nitafuta upanga nyuma yao.

13. Hivyo ndivyo ghadhabu yangu itakavyotimia, nami nitatosheleza hasira yangu juu yao, nami nitafarijika; nao watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimenena kwa wivu wangu, nitakapokuwa nimeitimiza ghadhabu yangu juu yao.

14. Tena nitakufanya kuwa ukiwa, na aibu, kati ya mataifa wakuzungukao, machoni pa watu wote wapitao.

15. Nayo itakuwa tukano na aibu, na mafundisho na ajabu, kwa mataifa wakuzungukao, hapo nitakapotekeleza hukumu ndani yako, kwa hasira, na kwa ghadhabu, na kwa malaumu ya ghadhabu; mimi, BWANA, nimeyanena hayo;

16. hapo nitakapopeleka mishale mibaya ya njaa juu yao, iletayo uharibifu, nitakayoipeleka ili kuwaharibu ninyi; nami nitaiongeza njaa juu yenu, na tegemeo lenu la mkate nitalivunja.

17. Nami nitapeleka juu yenu njaa na wanyama wabaya, nao watakunyang’anya watu wako; na tauni na damu zitapita ndani yako; nami nitauleta upanga juu yako; mimi BWANA, nimeyanena hayo.

Eze. 5