Eze. 46:12-24 Swahili Union Version (SUV)

12. Naye mkuu atakapotengeneza sadaka atoayo kwa hiari yake mwenyewe, sadaka ya kuteketezwa, au sadaka za amani, ziwe sadaka amtoleazo BWANA kwa hiari yake mwenyewe, mtu mmoja atamfungulia lango lile lielekealo upande wa mashariki, naye ataitengeneza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka zake za amani, kama afanyavyo siku ya sabato; kisha atatoka; na baada ya kutoka kwake mtu mmoja atalifunga lango.

13. Nawe utatengeneza mwana-kondoo wa mwaka wa kwanza, mkamilifu, kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA kila siku; kila siku asubuhi utamtengeneza.

14. Nawe utatengeneza sadaka ya unga pamoja nayo kila siku asubuhi, sehemu ya sita ya efa moja, na sehemu ya tatu ya hini moja ya mafuta; kuchanganya na unga ule mzuri; sadaka ya unga kwa BWANA daima, kwa amri ya milele.

15. Hivyo ndivyo watakavyomtengeneza mwana-kondoo, na sadaka ya unga, na mafuta, kila siku asubuhi, kuwa sadaka ya kuteketezwa ya daima.

16. Bwana MUNGU asema hivi; Mkuu akimpa mwanawe awaye yote zawadi, ni urithi wake, itakuwa mali ya wanawe; ni milki yao kwa kurithiwa.

17. Bali akimpa mmoja wa watumishi wake baadhi ya urithi wake, itakuwa mali yake mpaka mwaka wa kuacha huru; ndipo itakapomrudia mkuu; lakini urithi wake, huo utakuwa wa wanawe.

18. Tena mkuu hatawaondolea watu urithi wao, hata kuwatoa kwa nguvu katika milki yao; atawapa wanawe urithi katika mali yake mwenyewe, watu wangu wasije wakatawanyika, kila mtu mbali na milki yake.

19. Ndipo akanileta kati ya maingilio, yaliyokuwa kando ya lango, mpaka vyumba vitakatifu vya makuhani, vilivyoelekea upande wa kaskazini; na tazama, palikuwa na mahali, upande wa nyuma ulioelekea magharibi.

20. Akaniambia, Hapa ndipo mahali pa makuhani, watakapoitokosa sadaka ya hatia, na sadaka ya dhambi, watakapoioka sadaka ya unga; kusudi wasizilete nje katika ua wa nje, na kuwatakasa watu.

21. Kisha akanileta mpaka ua wa nje, akanipitisha karibu na pembe nne za ua huo; na tazama, katika kila pembe ya ua huo palikuwa na kiwanja.

22. Katika pembe nne za ua huo palikuwa na viwanja vilivyoungana, urefu wake dhiraa arobaini, na upana wake thelathini; viwanja hivyo vinne vya pembeni vilikuwa vya kipimo kimoja.

23. Tena palikuwa na safu ndani yake pande zote, kuvizunguka vile viwanja vinne; tena palifanywa meko ya kutokosea, chini ya safu pande zote.

24. Ndipo akaniambia, Hizi ni nyumba za kutokosea, ambamo wahudumu wa nyumba watatokosa sadaka za watu.

Eze. 46