1. Kisha akanileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki;
2. na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling’aa kwa utukufu wake.
3. Na maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona nilipokuja kuuharibu mji; nayo maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona karibu na mto wa Kebari; nikaanguka kifudifudi.
4. Na huo utukufu wa BWANA ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki.
5. Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa BWANA uliijaza nyumba.
6. Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami.
7. Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele; na nyumba ya Israeli hawatalinajisi jina langu takatifu tena, wao, wala wafalme wao, kwa mambo yao ya kikahaba, na kwa mizoga ya wafalme wao, katika mahali pao pa juu;