37. Na miimo yake iliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake, upande huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia.
38. Na chumba, pamoja na lango lake, kilikuwa karibu na miimo ya malango; ndiko walikoiosha sadaka ya kuteketezwa.
39. Na katika ukumbi wa lango palikuwa na meza mbili upande huu, na meza mbili upande huu, ili kuichinja sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia.
40. Na upande mmoja, nje, penye madaraja ya kuliingia lango lililoelekea kaskazini, palikuwa na meza mbili; na upande wa pili, ulio wa ukumbi wa lango hilo, palikuwa na meza mbili.
41. Palikuwa na meza nne upande huu, na meza nne upande huu, karibu na lango; meza nane ambazo juu yake walizichinja sadaka.
42. Tena palikuwa na meza nne kwa sadaka za kuteketezwa, za mawe yaliyochongwa; urefu wake dhiraa moja na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja; juu yake waliviweka vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na sadaka.
43. Tena hizo kulabu, ambazo urefu wake ni shubiri, zilifungwa ndani pande zote; na juu ya meza hizo ilikuwako nyama ya matoleo.
44. Tena nje ya lango la ndani palikuwa na vyumba kwa waimbaji, katika ua wa ndani, uliokuwa kando ya lango lililoelekea kaskazini, navyo vilikabili upande wa kusini; na kimoja kando ya lango lililoelekea upande wa mashariki, kilikabili upande wa kaskazini.
45. Akaniambia, Chumba hiki kinachokabili upande wa kusini ni kwa makuhani, yaani, hao walinzi wa malindo ya nyumba.
46. Nacho chumba kinachokabili upande wa kaskazini ni kwa makuhani, walinzi wa malindo ya madhabahu; hao ni wana wa Sadoki, ambao miongoni mwa wana wa Lawi wamkaribia BWANA, ili kumtumikia.
47. Akaupima huo ua, na urefu wake ulikuwa dhiraa mia, na upana wake dhiraa mia, mraba; nayo dhabahu ilikuwa mbele ya nyumba.
48. Ndipo akanileta mpaka ukumbi wa nyumba, akapima kila mwimo wa ukumbi, dhiraa tano upande huu, na dhiraa tano upande huu; na upana wa lango ulikuwa dhiraa tatu upande huu, na dhiraa tatu upande huu.
49. Urefu wa ukumbi ulikuwa dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi na moja; karibu na madaraja ambayo waliupandia; tena palikuwa na nguzo karibu na miimo, moja upande huu, na moja upande huu.