1. Katika mwaka wa ishirini na tano wa kuhamishwa kwetu, mwanzo wa mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kupigwa mji, siku iyo hiyo, mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, akanileta huko.
2. Katika maono ya Mungu alinileta mpaka nchi ya Israeli, akaniweka juu ya mlima mrefu sana, ambao juu yake palikuwapo kana kwamba ni umbo la mji upande wa kusini.
3. Akanileta huko, na tazama, alikuwapo mtu, ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba, naye alikuwa na uzi wa kitani mkononi mwake, na mwanzi wa kupimia; akasimama karibu na lango.
4. Mtu yule akaniambia, Mwanadamu, tazama kwa macho yako, sikia kwa masikio yako, ukaweke moyoni mwako, yote nitakayokuonyesha; maana umeletwa hapa kusudi nikuonyeshe haya; tangaza habari ya yote utakayoyaona kwa nyumba ya Israeli.
5. Na, tazama, kulikuwa na ukuta nje ya nyumba pande zote, na katika mkono wa mtu yule mwanzi wa kupimia, urefu wake dhiraa sita, kila dhiraa, dhiraa na shubiri; basi akaupima upana wa jengo lile, mwanzi mmoja, na urefu wake, mwanzi mmoja.
6. Kisha akaenda mpaka lango lielekealo upande wa mashariki, akapanda madaraja yake; akakipima kizingiti cha lango; upana wake mwanzi mmoja; na kizingiti cha pili, upana wake mwanzi mmoja.
7. Na kila chumba, upana wake mwanzi mmoja, na urefu wake mwanzi mmoja; na nafasi iliyokuwa kati ya vyumba ni dhiraa tano; na kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja.
8. Akaupima na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja.
9. Kisha akaupima ukumbi wa lango, dhiraa nane; na miimo yake, dhiraa mbili; na ukumbi wa lango uliielekea nyumba.
10. Na vyumba vya walinzi, vya lango upande wa mashariki, vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; vyote vitatu vya kipimo kimoja; nayo miimo ilikuwa na kipimo kimoja, upande huu na upande huu.
11. Akaupima upana wa mahali pa kuliingilia lango, dhiraa kumi; na urefu wa lango, dhiraa kumi na tatu.
12. Na mpaka, mbele ya vile vyumba, dhiraa moja upande huu, na mpaka, dhiraa moja upande huu; na vile vyumba, dhiraa sita upande huu, na dhiraa sita upande huu.