Eze. 36:20-34 Swahili Union Version (SUV)

20. Nao walipoyafikilia mataifa yale waliyoyaendea, walilitia unajisi jina langu takatifu; kwa kuwa watu waliwanena, wakisema, Watu hawa ni watu wa BWANA, nao wametoka katika nchi yake.

21. Lakini, naliwahurumia kwa ajili ya jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli walikuwa wamelitia unajisi katika mataifa waliyoyaendea.

22. Kwa hiyo; waambieni nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi Sitendi hili kwa ajili yenu, Ee nyumba ya Israeli, bali kwa ajili ya jina langu takatifu, mlilolitia unajisi katika mataifa mliyoyaendea.

23. Nami nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, asema Bwana MUNGU, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao.

24. Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe.

25. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote.

26. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.

27. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.

28. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

29. Nami nitawaokoeni na uchafu wenu wote; nitaiita ngano, na kuiongeza, wala sitaweka njaa juu yenu tena.

30. Nami nitazidisha matunda ya miti, na mazao ya mashamba, msipate tena kutukanwa na mataifa kwa sababu ya njaa.

31. Ndipo mtazikumbuka njia zenu mbaya, na matendo yenu yasiyokuwa mema, nanyi mtajichukia nafsi zenu kwa macho yenu, kwa sababu ya maovu yenu na machukizo yenu.

32. Ijulikane kwenu ya kuwa silitendi neno hili kwa ajili yenu, asema Bwana MUNGU; tahayarikeni, na kufadhaika, kwa sababu ya njia zenu, Enyi nyumba ya Israeli.

33. Bwana MUNGU asema hivi; Siku ile nitakapowatakaseni na maovu yenu yote, nitaifanya miji ikaliwe na watu, na palipobomolewa pajengwe tena.

34. Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa, ijapokuwa ilikuwa ukiwa mbele ya macho ya watu wote waliopita.

Eze. 36