15. kama mtu mwovu akirudisha rehani, na kumrudishia mtu mali yake aliyomnyang’anya, akizifuata sheria za uzima, asitende uovu wo wote; hakika ataishi, hatakufa.
16. Katika dhambi zake zote alizozitenda, hata mojawapo haitakumbukwa juu yake; ametenda yaliyo halali na haki; hakika ataishi.
17. Walakini wana wa watu wako husema, Njia ya Bwana si sawa; lakini watu hao, njia yao si sawa.
18. Mwenye haki ageukapo, na kuiacha haki yake, na kutenda maovu, atakufa katika maovu hayo.
19. Na mtu mbaya ageukapo, na kuuacha ubaya wake, na kutenda yaliyo halali na haki, ataishi kwa matendo hayo.
20. Lakini ninyi husema, Njia ya Bwana si sawa. Ee nyumba ya Israeli, nitawahukumu ninyi; kila mtu kwa kadiri ya njia zake.
21. Ikawa, katika mwaka wa kumi na mbili wa kuhamishwa kwetu, mwezi wa kumi, siku ya tano ya mwezi, mtu mmoja aliyekuwa ametoroka toka Yerusalemu akanijia, akisema, Mji umepigwa.
22. Basi mkono wa Bwana umekuwa juu yangu wakati wa jioni, kabla hajafika yeye aliyetoroka; naye alikuwa amenifumbua kinywa changu, hata aliponijia wakati wa asubuhi; na kinywa changu kilikuwa wazi, wala sikuwa bubu tena.
23. Neno la BWANA likanijia, kusema,
24. Mwanadamu, watu wale wakaao mahali palipoharibika katika nchi ya Israeli husema ya kwamba, Ibrahimu alikuwa mmoja, akairithi nchi hii; lakini sisi tu watu wengi; tumepewa nchi hii iwe urithi wetu.
25. Basi, waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Mnakula nyama pamoja na damu yake, na kuviinulia vinyago vyenu macho yenu, na kumwaga damu; je, mtaimiliki nchi hii?
26. Mnategemea upanga wenu, mnatenda machukizo, mnanajisi kila mtu mke wa jirani yake; je! Mtaimiliki nchi hii?
27. Hivi ndivyo utakavyowaambia, Bwana MUNGU asema hivi; Kama mimi niishivyo, hakika watu wale wakaao mahali palipoharibika wataanguka kwa upanga, naye mtu aliye katika uwanda, nitamtoa na kuwapa wanyama wakali, ili aliwe; na hao walio ndani ya ngome na mapango watakufa kwa tauni.
28. Nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, na kiburi cha uwezo wake kitakoma; nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa, asipite mtu.
29. Ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, kwa sababu ya machukizo yao yote waliyoyatenda.
30. Nawe, mwanadamu, wana wa watu wako husimulia habari zako karibu na kuta, na ndani ya milango ya nyumba zao, na kuambiana, kila mtu na ndugu yake, wakisema, Haya! Twende tukasikie ni neno gani hilo litokalo kwa BWANA.