13. Nimwambiapo mwenye haki, ya kwamba hakika ataishi; kama akiitumainia haki yake, akatenda uovu, basi katika matendo yake ya haki, hata mojawapo halitakumbukwa; bali katika uovu wake alioutenda, atakufa katika uovu huo.
14. Tena, nimwambiapo mtu mwovu, Hakika utakufa; kama akighairi, na kuiacha dhambi yake, na kutenda yaliyo halali na haki;
15. kama mtu mwovu akirudisha rehani, na kumrudishia mtu mali yake aliyomnyang’anya, akizifuata sheria za uzima, asitende uovu wo wote; hakika ataishi, hatakufa.
16. Katika dhambi zake zote alizozitenda, hata mojawapo haitakumbukwa juu yake; ametenda yaliyo halali na haki; hakika ataishi.
17. Walakini wana wa watu wako husema, Njia ya Bwana si sawa; lakini watu hao, njia yao si sawa.
18. Mwenye haki ageukapo, na kuiacha haki yake, na kutenda maovu, atakufa katika maovu hayo.
19. Na mtu mbaya ageukapo, na kuuacha ubaya wake, na kutenda yaliyo halali na haki, ataishi kwa matendo hayo.
20. Lakini ninyi husema, Njia ya Bwana si sawa. Ee nyumba ya Israeli, nitawahukumu ninyi; kila mtu kwa kadiri ya njia zake.
21. Ikawa, katika mwaka wa kumi na mbili wa kuhamishwa kwetu, mwezi wa kumi, siku ya tano ya mwezi, mtu mmoja aliyekuwa ametoroka toka Yerusalemu akanijia, akisema, Mji umepigwa.
22. Basi mkono wa Bwana umekuwa juu yangu wakati wa jioni, kabla hajafika yeye aliyetoroka; naye alikuwa amenifumbua kinywa changu, hata aliponijia wakati wa asubuhi; na kinywa changu kilikuwa wazi, wala sikuwa bubu tena.
23. Neno la BWANA likanijia, kusema,
24. Mwanadamu, watu wale wakaao mahali palipoharibika katika nchi ya Israeli husema ya kwamba, Ibrahimu alikuwa mmoja, akairithi nchi hii; lakini sisi tu watu wengi; tumepewa nchi hii iwe urithi wetu.