33. Utajazwa ulevi na sikitiko, kwa kikombe cha ushangao na ukiwa, kikombe cha umbu lako Samaria.
34. Naam, utakinywea hata hakitabaki kitu ndani yake, utavitafuna vigae vyake, utayararua maziwa yako; maana mimi, Bwana MUNGU, nimenena neno hili.
35. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umenisahau, na kunitupa nyuma yako, basi kwa hiyo, uchukue uasherati wako na uzinzi wako.
36. Tena BWANA akaniambia, Mwanadamu, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi uwahubiri machukizo yao.
37. Maana wamezini, na damu imo mikononi mwao, nao wamezini na vinyago vyao; tena wana wao walionizalia wamewapitisha katika moto ili waliwe nao.
38. Tena wamenitenda haya; wamepatia unajisi mahali pangu patakatifu, siku ile ile, nao wamezitangua sabato zangu.
39. Kwa maana walipokuwa wamekwisha kuvichinjia vinyago vyao watoto wao, ndipo walipoingia patakatifu pangu, siku ile ile, wapatie unajisi, na tazama, wamefanya hivyo kati ya nyumba yangu.
40. Tena mmewatuma watu kuwaita watokao mbali; ambao mjumbe alitumwa kwao, na tazama, wakaja; nawe ulijiosha kwa ajili yao, ulitia rangi macho yako, na kujipamba vyombo vya uzuri;
41. ukaketi juu ya kitanda cha enzi, na meza imeandikwa tayari mbele yake, ambayo juu yake uliweka uvumba wangu na mafuta yangu.
42. Na sauti za wingi wa watu wenye hali ya raha zilikuwa pamoja naye; na pamoja na watu wasio na adabu, waliletwa walevi toka jangwani; wakawatia vikuku mikononi, na taji nzuri juu ya vichwa vyao.
43. Ndipo nikasema, Huyo aliye mkongwe atafanya uzinzi! Sasa hao watazini naye, naam, na yeye!
44. Wakamwingilia kama watu wamwingiliavyo kahaba; ndivyo walivyowaingilia Ohola na Oholiba, wanawake wale waasherati.
45. Basi watu wenye haki watawahukumu, kwa hukumu iwapasayo wazinzi, na kwa hukumu iwapasayo wanawake wamwagao damu; kwa sababu wao ndio wazinzi, na mikononi mwao mna damu.
46. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitaleta kusanyiko la watu juu yao, nami nitawatoa warushwe huko na huko, na kutekwa nyara.