Eze. 20:6-23 Swahili Union Version (SUV)

6. katika siku ile naliwainulia mkono wangu, kuwatoa katika nchi ya Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyowapelelezea, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote;

7. nikawaambia, Kila mtu kwenu na atupilie mbali machukizo ya macho yake, wala msijitie unajisi kwa vinyago vya Misri, Mimi ni BWANA, Mungu wenu.

8. Lakini waliniasi, wala hawakutaka kunisikiliza; hawakutupilia mbali kila mtu machukizo ya macho yake, wala hawakuviacha vinyago vya Misri; ndipo nikasema kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao, katikati ya nchi ya Misri.

9. Lakini nalitenda kwa ajili ya jina langu, ili lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao walikaa pamoja nao, ambao machoni pao nalijidhihirisha kwao, kwa kuwatoa katika nchi ya Misri.

10. Basi nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta jangwani.

11. Nikawapa amri zangu, na kuwaonyesha hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda.

12. Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye.

13. Lakini nyumba ya Israeli waliniasi jangwani; hawakuenda katika amri zangu, wakazikataa hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda; na sabato zangu walizitia unajisi sana; ndipo nikasema, Nitamwaga hasira yangu juu yao jangwani, ili niwaangamize.

14. Lakini nalitenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi machoni pa mataifa, ambao naliwatoa mbele ya macho yao.

15. Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, ya kwamba sitawaingiza katika nchi ile niliyokuwa nimewapa, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote;

16. kwa sababu walizikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika amri zangu, wakazitia unajisi sabato zangu, kwa maana mioyo yao iliandama vinyago vyao.

17. Walakini jicho langu likawahurumia nisiwaangamize kabisa, wala sikuwakomesha kabisa jangwani.

18. Kisha nikawaambia watoto wao jangwani, Msiende katika amri za baba zenu, wala msizishike hukumu zao, wala msijitie unajisi kwa vinyago vyao.

19. Mimi ni BWANA, Mungu wenu; endeni katika amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzitenda;

20. zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.

21. Lakini watoto hao waliniasi; hawakuenda katika amri zangu, wala hawakuzishika hukumu zangu kuzitenda, ambazo mwanadamu ataishi kwazo kama akizitenda; walizitia unajisi sabato zangu, ndipo nikasema, kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao jangwani.

22. Lakini naliuzuia mkono wangu, nikatenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao mbele ya macho yao naliwatoa.

23. Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, kwamba nitawatawanya kati ya mataifa, na kuwatapanya katika nchi mbalimbali;

Eze. 20