11. wala hakutenda mojawapo la mambo hayo yampasayo, bali amekula juu ya milima, na kumtia unajisi mke wa jirani yake,
12. na kuwadhulumu maskini na wahitaji, na kuwanyang’anya watu mali yao kwa nguvu, wala hakurudisha rehani, naye ameviinulia macho vinyago, na kufanya machukizo,
13. naye amekopesha watu ili apate faida, na kupokea ziada; je! Ataishi baada ya hayo? La, hataishi; amefanya machukizo hayo yote; hakika atakufa; damu yake itakuwa juu yake.
14. Na kama yeye huyo akizaa mwana, naye ameona dhambi zote za baba yake alizozitenda, akaogopa, asifanye neno lo lote kama hayo;
15. hakula juu ya milima, wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa jirani yake,
16. wala hakumdhulumu mtu, wala hakutwaa kitu kiwekwe rehani, wala hakumnyang’anya mtu mali yake kwa nguvu, bali amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwafunika nguo walio uchi;
17. tena ikiwa ameuzuia mkono wake asimwonee maskini, wala hakupokea faida na ziada, naye amezifanya hukumu zangu, na kuzifuata sheria zangu; hatakufa huyu kwa sababu ya uovu wa baba yake, hakika ataishi.
18. Kwa habari za yule baba yake, kwa sababu aliwaonea watu kwa ukali mwingi, na kumnyang’anya ndugu yake mali yake kwa nguvu; na kuyatenda yasiyo mema kati ya watu wake, tazama, atakufa katika uovu wake.