37. basi, tazama, nitawakusanya wapenzi wako wote ambao umejifurahisha pamoja nao, nao wote uliowapenda, pamoja na watu wote uliowachukia; naam, nitawakusanya juu yako pande zote, na kuwafunulia uchi wako, wapate kuuona uchi wako wote.
38. Nami nitakuhukumu, kama wahukumiwavyo wake walioolewa wazinio, na kumwaga damu, nami nitakupatiliza damu ya ghadhabu na wivu.
39. Tena nitakutia katika mikono yao, nao watapaangusha mahali pako pakuu, na kupabomoa mahali pako palipoinuka, nao watakuvua nguo zako, na kutwaa vyombo vyako vya uzuri, nao watakuacha uchi, huna nguo.
40. Tena wataleta mkutano wa watu juu yako, nao watakupiga kwa mawe, na kukuchoma kwa panga zao.
41. Nao watazipiga moto nyumba zako, na kutekeleza hukumu juu yako mbele ya wanawake wengi, nami nitakulazimisha kuacha mambo ya kikahaba, wala hutatoa ujira tena.
42. Hivyo ndivyo nitakavyoshibisha ghadhabu yangu juu yako, na wivu wangu utanitoka, nami nitatulia wala sitaona hasira tena.
43. Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako, bali umenikasirisha kwa mambo hayo yote; basi, tazama, mimi nami nitaleta njia yako juu ya kichwa chako, asema Bwana MUNGU; wala hutafanya uasherati zaidi ya machukizo yako yote.
44. Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia mithali hii kinyume chako, akisema, Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake.
45. Wewe u binti ya mama yako, amchukiaye mume wake na watoto wake; nawe u umbu la maumbu yako, waliowachukia waume zao na watoto wao; mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako Mwamori.
46. Na umbu lako mkubwa ni Samaria, akaaye mkono wako wa kushoto, yeye na binti zake; na umbu lako mdogo, akaaye mkono wako wa kuume, ni Sodoma na binti zake.
47. Lakini hukuenda katika njia zao, wala hukutenda sawasawa na machukizo yao; lakini kana kwamba hilo ni jambo dogo sana, ulikuwa umeharibika kuliko wao katika njia zako zote.