13. Hivyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha; na mavazi yako yalikuwa ya kitani safi, na hariri, na kazi ya taraza; ulikula unga mzuri, na asali, na mafuta; nawe ulikuwa mzuri mno, ukafanikiwa hata kufikilia hali ya kifalme.
14. Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kwa sababu ya uzuri wako; kwa maana ulikuwa mkamilifu, kwa sababu ya utukufu wangu niliokutia, asema Bwana MUNGU.
15. Lakini uliutumainia uzuri wako, ukafanya mambo ya kikahaba kwa sababu ya sifa zako, ukamwaga mambo yako ya kikahaba juu ya kila mtu aliyepita; ulikuwa wake.
16. Ukatwaa baadhi ya mavazi yako, ukajifanyia mahali palipoinuka, palipopambwa kwa rangi mbalimbali, ukafanya mambo ya kikahaba juu yake; mambo kama hayo hayatakuja wala hayatakuwako.
17. Pia ulivitwaa vyombo vyako vya uzuri, vya dhahabu yangu na vya fedha yangu, nilivyokupa, ukajifanyia sanamu za wanaume, ukafanya mambo ya kikahaba pamoja nazo;
18. ukatwaa nguo zako za kazi ya taraza, ukawafunika, ukaweka mafuta yangu na uvumba wangu mbele yao.
19. Mkate wangu niliokupa, unga mzuri, na mafuta, na asali, nilivyokulisha, ukaviweka mbele yao viwe harufu ya kupendeza; na ndivyo vilivyokuwa; asema Bwana MUNGU.
20. Pamoja na hayo uliwatwaa wana wako na binti zako, ulionizalia, ukawatoa sadaka kwao ili waliwe. Je! Mambo yako ya kikahaba ni kitu kidogo tu,
21. hata ukawaua watoto wangu, na kuwatoa kwa kuwapitisha motoni kwa hao?
22. Na katika machukizo yako yote, na mambo yako ya kikahaba, hukuzikumbuka siku za ujana wako, ulipokuwa uchi, huna nguo, ukawa ukigaagaa katika damu yako.