Eze. 14:8-20 Swahili Union Version (SUV)

8. nami nitaukaza uso wangu juu ya mtu yule, na kumfanya kuwa ajabu, awe ishara na mithali, nami nitamkatilia mbali, asiwe kati ya watu wangu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

9. Na nabii akidanganyika, na kusema neno, mimi, BWANA, nimemdanganya nabii yule, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli.

10. Nao watauchukua uovu wao; uovu wa nabii utakuwa sawasawa na uovu wake yule amwendeaye aulize neno;

11. ili nyumba ya Israeli wasipotee mbali nami, wala wasijitie unajisi tena kwa makosa yao yote; bali wawe watu wangu, nami niwe Mungu wao, asema Bwana MUNGU.

12. Neno la BWANA likanijia, kusema,

13. Mwanadamu, nchi itakapofanya dhambi na kuniasi, kwa kukosa, nikaunyosha mkono wangu juu yake, na kulivunja tegemeo la chakula chake, na kuipelekea njaa, na kukatilia mbali mwanadamu na mnyama;

14. wajapokuwa watu hawa watatu, Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kuwamo ndani yake, wangejiokoa nafsi zao wenyewe tu kwa haki yao, asema Bwana MUNGU.

15. Nikipitisha wanyama wabaya ndani ya nchi ile, wakaiharibu hata ikawa ukiwa, mtu awaye yote asiweze kupita ndani yake, kwa sababu ya wanyama hao;

16. wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; wao wenyewe tu wataokoka, bali nchi ile itakuwa ukiwa.

17. Au nikileta upanga juu ya nchi ile, na kusema, Upanga, pita kati ya nchi hii, hata nikawakatilia mbali na nchi hiyo wanadamu na wanyama;

18. wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; bali wao wenyewe tu wataokoka.

19. Au nikipeleka tauni katika nchi ile, na kumwaga ghadhabu yangu juu yake, kwa damu; ili kuwakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama;

20. wajapokuwamo ndani yake Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; watajiokoa nafsi zao tu kwa haki yao.

Eze. 14