Eze. 11:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. Tena roho ikaniinua, ikanileta hata lango la upande wa mashariki wa nyumba ya BWANA, lililoelekea upande wa mashariki; na tazama, mahali pa kuingilia pa lango walikuwako watu ishirini na watano; na katikati yao nikamwona Yaazania, mwana wa Azuri, na Pelatia, mwana wa Benaya, nao ni wakuu wa watu.

2. Akaniambia, Mwanadamu, hawa ndio watu wale watungao uovu, na kutoa mashauri mabaya ndani ya mji huu;

3. wasemao, Wakati wa kujenga nyumba si karibu; mji huu ni sufuria na sisi ni nyama.

4. Basi toa unabii juu yao, Ee mwanadamu, toa unabii.

5. Roho ya BWANA ikaniangukia, naye akaniambia, Nena, BWANA asema hivi; Mmesema maneno hayo, Enyi nyumba ya Israeli; maana mimi nayajua yaingiayo katika mioyo yenu.

6. Mmewaongeza watu wenu waliouawa ndani ya mji wenu, nanyi mmezijaza njia kuu zake waliouawa.

7. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Watu wenu waliouawa, ambao mmewalaza katikati yake, hao ndio nyama hiyo, na mji huu ndio sufuria; lakini ninyi mtatolewa nje kutoka katikati yake.

8. Ninyi mmeuogopa upanga; nami nitauleta upanga juu yenu, asema Bwana MUNGU.

9. Nami nitawatoa ninyi nje kutoka katikati yake, na kuwatia katika mikono ya wageni, nami nitafanya hukumu kati yenu.

10. Mtaanguka kwa upanga; nitawahukumu katika mpaka wa Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

Eze. 11