12. Mfalme akamwambia malkia Esta, Wayahudi wamewaua watu mia tano hapa Shushani ngomeni na kuwaangamiza, pamoja na wana kumi wa Hamani, je! Wamefanyaje basi katika majimbo ya mfalme yaliyosalia! Basi, una nini uombalo? Nawe utapewa; ama unayo haja gani tena? Nayo itatimizwa.
13. Ndipo Esta aliposema, Mfalme akiona vema, Wayahudi walioko Shushani na wapewe ruhusa kufanya tena kesho sawasawa na mbiu ya leo, na hao wana kumi wa Hamani watundikwe juu ya mti ule.
14. Mfalme akaamuru vifanyike vivyo hivyo, mbiu ikapigwa huko Shushani, wakawatundika wale wana kumi wa Hamani.
15. Basi Wayahudi wa Shushani wakakusanyika tena siku ya kumi na nne pia ya mwezi wa Adari, wakawaua watu mia tatu huko Shushani; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono.
16. Nao Wayahudi wengine waliokaa katika majimbo ya mfalme walikusanyika, wakazishindania maisha zao, wakajipatia raha mbele ya adui zao, wakawaua waliowachukia, watu sabini na tano elfu; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono.
17. Hii ndiyo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari; na siku ya kumi na nne ya mwezi huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha.
18. Lakini Wayahudi wa Shushani walikusanyika siku ya kumi na tatu ya mwezi huo, na siku ya kumi na nne pia; na siku ya kumi na tano ya mwezi uo huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha.
19. Kwa sababu hii Wayahudi wa vijijini, wakaao katika miji isiyo na boma, huishika siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, kuwa siku ya furaha na karamu, sikukuu ya kupelekeana zawadi.
20. Basi Mordekai aliyaandika mambo hayo; naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote waliokaa katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero, waliokuwa karibu na waliokuwa mbali,
21. kuwaonya wazishike siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, na siku ya kumi na tano yake, mwaka kwa mwaka,
22. ambazo ni siku Wayahudi walipojipatia raha mbele ya adui zao, na mwezi uliogeuzwa kwao kuwa furaha badala ya huzuni, na kuwa sikukuu badala ya kilio; wazifanye siku hizo ziwe za karamu na furaha, za kupeana zawadi na za kuwapa maskini vipawa.