13. Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme.
14. Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?
15. Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu?
16. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili.
17. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme.
18. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
19. Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto.
20. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.
21. Basi watu hao wakafungwa, hali wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.
22. Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego.
23. Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto.
24. Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme.
25. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.