7. Nami, Danieli, nikaona maono haya peke yangu; maana wale watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona maono haya; lakini tetemeko kuu liliwashika, hata wakakimbia ili kujificha.
8. Basi nikaachwa peke yangu, nikaona maono haya makubwa, wala hazikubaki nguvu ndani yangu; maana uzuri wangu uligeuzwa ndani yangu kuwa uharibifu, wala sikusaziwa nguvu.
9. Walakini naliisikia sauti ya maneno yake; nami niliposikia sauti ya maneno yake, ndipo nikashikwa na usingizi mzito, na uso wangu umeielekea nchi.
10. Na tazama, mkono ukanigusa, ukaniweka juu ya magoti yangu, na vitanga vya mikono yangu.
11. Akaniambia, Ee Danieli, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima; maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia neno hili, nalisimama nikitetemeka.
12. Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako.
13. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.
14. Sasa nimekuja kukufahamisha mambo yatakayowapata watu wako katika siku za mwisho; maana maono hayo ni ya siku nyingi bado.
15. Na alipokwisha kusema nami maneno hayo, nikauelekeza uso wangu chini, nikawa bubu.