1. Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, Danieli, ambaye jina lake aliitwa Belteshaza, alifunuliwa neno; na neno lile lilikuwa kweli; maana ni vita vikubwa; naye akalifahamu neno lile, akaelewa na maono hayo.
2. Katika siku zile mimi, Danieli, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili.
3. Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia.
4. Na siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa kando ya ule mto mkubwa, Hidekeli;
5. naliinua macho yangu, nikatazama, na kumbe, mtu aliyevikwa nguo za kitani, viuno vyake vimefungwa dhahabu safi ya Ufazi;
6. mwili wake pia ulikuwa kama zabarajadi safi, na uso wake mfano wa umeme, na macho yake kama taa za moto, na mikono yake na miguu yake rangi yake kama shaba iliyosuguliwa sana, na sauti ya maneno yake kama sauti ya umati wa watu.
7. Nami, Danieli, nikaona maono haya peke yangu; maana wale watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona maono haya; lakini tetemeko kuu liliwashika, hata wakakimbia ili kujificha.
8. Basi nikaachwa peke yangu, nikaona maono haya makubwa, wala hazikubaki nguvu ndani yangu; maana uzuri wangu uligeuzwa ndani yangu kuwa uharibifu, wala sikusaziwa nguvu.