Ayu. 38:19-30 Swahili Union Version (SUV)

19. Iko wapi njia ya kuyafikia makao ya nuru?Na giza pia, mahali pake ni wapi?

20. Upate kuipeleka hata mpaka wake,Upate kuelewa na mapito ya kuiendea nyumba yake?

21. Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo,Na hesabu ya siku zako ni kubwa!

22. Je! Umeziingia ghala za theluji,Au umeziona ghala za mvua ya mawe,

23. Nilizoziweka akiba kwa wakati wa misiba,Kwa siku ya mapigano na vita?

24. Je! Nuru hutengwa kwa njia gani,Au upepo wa mashariki hutawanywaje juu ya nchi?

25. Ni nani aliyepasua mfereji kwa maji ya gharika,Au njia kwa umeme wa radi;

26. Kunyesha mvua juu ya nchi isiyo na watu;Juu ya jangwa asiyokaa mwanadamu;

27. Kuishibisha nchi iliyo kame na ukiwa,Na kuyameza majani yaliyo mororo?

28. Je! Mvua ina baba?Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande?

29. Barafu ilitoka katika tumbo la nani?Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa?

30. Maji hugandamana kama jiwe,Na uso wa vilindi huganda kwa baridi.

Ayu. 38