Ayu. 20:6-25 Swahili Union Version (SUV)

6. Ujapopanda ukuu wake mpaka mbinguni,Na kichwa chake kufikilia mawinguni;

7. Hata hivyo ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe;Hao waliomwona watasema, Yuko wapi?

8. Ataruka mfano wa ndoto, asionekane;Naam, atafukuzwa kama maono ya usiku,

9. Jicho lililomwona halitamwona tena;Wala mahali pake hapatamtazama tena.

10. Watoto wake watataka fadhili kwa maskini,Na mikono yake itarudisha mali yake.

11. Mifupa yake imejaa ujana wake,Lakini utalala nchi naye mavumbini.

12. Ingawa uovu una tamu kinywani mwake,Ingawa auficha chini ya ulimi wake;

13. Ingawa auhurumia, asikubali kuuacha uende zake.Lakini akaushika vivyo kinywani mwake;

14. Hata hivyo chakula chake matumboni mwake kinabadilika,Kimekuwa ni nyongo za majoka ndani yake.

15. Amemeza mali, naye atayatapika tena;Mungu atayatoa tumboni mwake.

16. Ataamwa sumu ya majoka;Na ulimi wa fira utamwua.

17. Hataiangalia hiyo mito ya maji,Vile vijito vilivyojaa asali na siagi.

18. Aliyoyataabikia kazi atayarudisha, asiyameze;Kwa mali aliyoyapata, hatafurahi.

19. Kwa maana amewaonea na kuwaacha maskini;Amenyang’anya nyumba kwa jeuri, wala hataijenga.

20. Kwa sababu hakujua utulivu ndani yake,Hataponya cho chote katika hicho alichokifurahia.

21. Hakikusalia kitu asichokula;Kwa hiyo kufanikiwa kwake hakutadumu.

22. Katika kujaa kwa wingi wake atakuwa katika dhiki;Mkono wa kila anayesumbuliwa utamjia.

23. Hapo atakapo kulijaza tumbo lake,Mungu atamtupia ukali wa ghadhabu zake,Na kuunyesha juu yake akiwa anakula.

24. Ataikimbia silaha ya chuma,Na uta wa shaba utamchoma kwa pili.

25. Yeye autoa, nao watoka mwilini mwake;Naam, ncha ing’aayo yatoka katika nyongo yake;Vitisho viko juu yake.

Ayu. 20