6. Hao wakuu wa Sukothi wakasema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna i mkononi mwako sasa, hata sisi tukawape jeshi lako mikate?
7. Ndipo Gideoni akasema, Kwa sababu hii, hapo BWANA atakapokuwa amewatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, ndipo nitaipura nyama ya miili yenu kwa miiba ya nyikani, na kwa michongoma.
8. Basi kutoka hapo alikwea kwenda Penieli, akasema na watu wa mahali hapo maneno kama hayo; watu wa Penieli nao wakamjibu kama vile watu wa Sukothi walivyomjibu.
9. Naye akawaambia hao watu wa Penieli nao, akisema, Nitakapokuja tena kwa amani, nitauvunja mnara huu.
10. Basi hao kina Zebu na Salmuna walikuwa katika Karkori, na majeshi yao walikuwa pamoja nao, watu kama kumi na tano elfu hesabu yao, ni wote waliobaki wa hilo jeshi lote la hao wana wa mashariki; kwa sababu walianguka watu mia na ishirini elfu waliokuwa wenye kutumia upanga.
11. Basi Gideoni alikwea kwa njia ya hao waliokuwa wenye kukaa hemani upande wa mashariki wa Noba na Yogbeha, akalipiga hilo jeshi; kwa maana lile jeshi lilikuwa salama.
12. Zeba na Salmuna walikimbia; naye akawaandamia; akawakamata hao wafalme wawili wa Midiani Zeba na Salmuna, akalitapanya-tapanya hilo jeshi lote.
13. Kisha huyo Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani, kutoka kwenye makweleo ya Heresi.
14. Ndipo akamshika mtu mmoja hirimu katika watu wa Sukothi, akamwuliza; naye akamwandikia majina ya hao wakuu wa Sukothi, na wazee wa mji, watu sabini na saba.
15. Kisha akawafikilia wale watu wa Sukothi, akawaambia, Tazama, Zeba na Salmuna, ambao ninyi mlinisimanga kwa ajili yao, mliposema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna iko sasa mikononi mwako wewe, hata tuwape watu wako waliochoka mikate?
16. Basi akawatwaa hao wazee wa mji, na miiba ya nyikani na michongoma, akawafunza hao watu wa Sukothi kwayo.
17. Kisha akaupomosha mnara wa Penieli, na kuwaua watu wa mji huo.
18. Ndipo akawaambia hao Zeba na Salmuna, Hao watu mliowaua huko Tabori walikuwa watu wa namna gani? Wakamjibu, Walikuwa kama wewe ulivyo; kila mmoja alikuwa anafanana na wana wa mfalme.
19. Naye akasema, Watu hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mamaangu mimi; kama yeye BWANA alivyo hai, kwamba mliwaokoa hai watu hao, mimi nisingewaua ninyi.
20. Kisha akamwambia Yetheri mwanawe mzaliwa wa kwanza, Haya, simama, uwaue hawa. Lakini huyo kijana hakutoa upanga wake; maana, akacha, kwa sababu alikuwa ni kijana tu.
21. Ndipo hapo Zeba na Salmuna wakasema, Simama wewe ukatuangukie sisi; kwa maana kama mtu alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake. Basi Gideoni akasimama, akawaua Zeba na Salmuna, akazitwaa koja zilizokuwa katika shingo za ngamia zao.
22. Ndipo watu wa Israeli wakamwambia Gideoni, Tawala wewe juu yetu, wewe, na mwanao, na mjukuu wako pia; kwa kuwa wewe umetuokoa na mikono ya Midiani.