Amu. 8:18-29 Swahili Union Version (SUV)

18. Ndipo akawaambia hao Zeba na Salmuna, Hao watu mliowaua huko Tabori walikuwa watu wa namna gani? Wakamjibu, Walikuwa kama wewe ulivyo; kila mmoja alikuwa anafanana na wana wa mfalme.

19. Naye akasema, Watu hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mamaangu mimi; kama yeye BWANA alivyo hai, kwamba mliwaokoa hai watu hao, mimi nisingewaua ninyi.

20. Kisha akamwambia Yetheri mwanawe mzaliwa wa kwanza, Haya, simama, uwaue hawa. Lakini huyo kijana hakutoa upanga wake; maana, akacha, kwa sababu alikuwa ni kijana tu.

21. Ndipo hapo Zeba na Salmuna wakasema, Simama wewe ukatuangukie sisi; kwa maana kama mtu alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake. Basi Gideoni akasimama, akawaua Zeba na Salmuna, akazitwaa koja zilizokuwa katika shingo za ngamia zao.

22. Ndipo watu wa Israeli wakamwambia Gideoni, Tawala wewe juu yetu, wewe, na mwanao, na mjukuu wako pia; kwa kuwa wewe umetuokoa na mikono ya Midiani.

23. Gideoni akawaambia, Mimi sitatawala juu yenu wala mwanangu hatatawala juu yenu; yeye BWANA atatawala juu yenu.

24. Kisha Gideoni akawaambia, Mimi nina haja yangu niitakayo kwenu, ni ya kila mtu kunipa hizo pete za masikio ya mateka yake. (Kwa maana walikuwa na pete za masikio za dhahabu, kwa sababu walikuwa ni Waishmaeli.)

25. Wakajibu, Tutakupa kwa mioyo. Basi wakatandika nguo chini, wakatia humo kila mtu pete za masikio ya mateka yake.

26. Na uzani wa hizo pete za dhahabu alizozitaka ulipata shekeli za dhahabu elfu moja na mia saba; mbali na makoja na vidani, na mavazi ya rangi ya zambarau waliyokuwa wameyavaa hao wafalme wa Midiani, tena mbali na mikufu iliyokuwa katika shingo za ngamia zao.

27. Basi Gideoni akafanya naivera kwa vitu vile, akaiweka katika mji wake, mji huo wa Ofra; nao Israeli wote wakaenda na kuiandama kwa ukahaba huko; nayo ilikuwa ni tanzi kwa Gideoni na kwa nyumba yake.

28. Hivyo Midiani walishindwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arobaini katika siku za Gideoni.

29. Kisha huyo Yerubaali, mwana wa Yoashi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe.

Amu. 8