Amu. 6:8-15 Swahili Union Version (SUV)

8. BWANA akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli; naye akawaambia, BWANA, yeye Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa;

9. nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri, na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, nami niliwapa ninyi nchi yao;

10. kisha niliwaambia, Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu; msiiche miungu ya Waamori, ambayo mwaketi katika nchi yao; lakini hamkuitii sauti yangu.

11. Malaika wa BWANA akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani.

12. Malaika wa BWANA akamtokea, akamwambia, BWANA yu pamoja nawe, Ee shujaa.

13. Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani.

14. BWANA akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma?

15. Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.

Amu. 6