6. Huyo akatuma mtu akamwita Baraka wa Abinoamu toka Kedesh-Naftali, akamwambia, Je! BWANA, Mungu wa Israeli, hakutoa amri, akisema, Enenda, ukawavute kwako, huko katika mlima wa Tabori, watu elfu kumi wa wana wa Naftali, na wa wana wa Zabuloni?
7. Nami nitakuvutia Sisera, amiri wa jeshi lake Yabini, hata mto wa Kishoni, pamoja na magari yake, na wingi wa watu wake; nami nitamtia mkononi mwako.
8. Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi.
9. Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana BWANA atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi.
10. Baraka akawakutanisha Naftali na Zabuloni waende Kedeshi wakakwea watu elfu kumi wakimfuata; Debora naye akaenda pamoja naye.
11. Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni, yaani na wana wa Hobabu, shemeji yake Musa, akaipiga hema yake mbali penye mwaloni ulioko Saanaimu, karibu na Kedeshi.
12. Watu wakamwambia Sisera ya kwamba Baraka, mwana wa Abinoamu amekwea kwenda mlima wa Tabori.