Amu. 3:19-31 Swahili Union Version (SUV)

19. Lakini yeye mwenyewe akageuka kutoka huko kwenye sanamu zilizokuwa karibu na Gilgali, akasema, Mimi nina ujumbe wa siri kwako wewe, Ee mfalme. Naye akasema, Nyamazeni kimya. Watu wote waliokuwa wanasimama karibu naye wakatoka na kumwacha.

20. Basi Ehudi akamwendea; naye alikuwa anaketi peke yake katika chumba chake cha baridi. Ehudi akasema, Mimi nina ujumbe utokao kwa Mungu kwako wewe. Basi akainuka katika kiti chake.

21. Ehudi akaunyosha mkono wake wa kushoto, akaushika huo upanga kuutoa hapo katika paja lake la kuume, akamtia tumboni mwake;

22. hicho kipini nacho kikaingia ndani pamoja na huo upanga wenyewe; nayo mafuta yakashikamana tena juu ya upanga, kwani hakuutoa tena upanga tumboni; nao ukatokea kwa nyuma.

23. Ndipo Ehudi akatoka nje barazani, akamfungia milango ya hicho chumba na kuifunga kwa ufunguo.

24. Basi alipokuwa amekwisha toka nje, hao watumishi wake wakaenda; wakaona, na tazama, hiyo milango ya chumba ilikuwa imefungwa kwa ufunguo; nao wakasema, Hapana budi amejifunika miguu yake ndani ya chumba cha baridi.

25. Wakangoja hata wakatahayari; na tazama, hakuifungua milango ya chumba; basi wakatwaa ufunguo, na kuifungua; na tazama, bwana wao alikuwa ameanguka nchi, naye amekufa.

26. Naye Ehudi alikimbia hapo walipokuwa wakingoja, akapita huko kwenye sanamu, na kukimbilia Seira.

27. Ikawa, hapo alipofika akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, ndipo wana wa Israeli wakatelemka pamoja naye kutoka huko milimani, naye akawatangulia.

28. Akawaambia, Niandameni mimi; kwa kuwa BWANA amewatia adui zenu, Wamoabi, mikononi mwenu. Basi wakatelemka na kumfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha Wamoabi, wala hawakumwacha mtu kuvuka.

29. Wakati huo wakapiga katika Wamoabi watu waume wapata kama elfu kumi, ambao wote walikuwa wanene, na wote mashujaa; hakupona hata mtu mmoja.

30. Basi Moabu alishindwa siku hiyo chini ya mikono ya Israeli. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka themanini

31. Tena baada yake huyo alikuwapo Shamgari mwana wa Anathi, aliyepiga katika Wafilisti watu mia sita kwa konzo la ng’ombe; yeye naye aliwaokoa Israeli.

Amu. 3