Amu. 21:7-21 Swahili Union Version (SUV)

7. Tufanyeje sisi ili tuwapatie wake hao waliosalia, kwa kuwa tumeapa kwa BWANA ya kwamba hatutawapa binti zetu ili wawaoe?

8. Basi wakasema, Ni ipi katika kabila za Israeli ambayo haikufika mbele ya BWANA huko Mispa? Na tazama, hakuja mmoja maragoni aliyetoka Yabeshi gileadi aufikilie huo mkutano.

9. Kwa maana hapo watu walipohesabiwa, hakuwapo hata mtu mmoja katika wenyeji wa Yabesh-gileadi.

10. Basi mkutano walipeleka huko watu kumi na mbili elfu wa hao waliokuwa mashujaa sana, kisha wakawaamuru, wakisema, Endeni mkawapige wenyeji wa Yabesh-gileadi kwa makali ya upanga, na hata wanawake na watoto wadogo.

11. Na jambo mtakalotenda ni hili; mtamwangamiza kila mume kabisa, na kila mwanamke ambaye amelala na mume.

12. Nao wakapata katika wenyeji wa Yabesh-gileadi wanawali mia nne, ambao hawajamjua mtu mume kwa kulala naye; basi wakawaleta maragoni huko Shilo, ulioko katika nchi ya Kanaani.

13. Basi mkutano ukatuma watu na kunena na wana wa Benyamini waliokuwako huko katika jabali la Rimoni, wakawatangazia amani.

14. Basi Benyamini wakarudi wakati huo; nao wakawapa wale wanawake waliowaponya wali hai katika hao wanawake wa Yabesh-gileadi; lakini hawakuwatosha.

15. Nao watu wakaghairi kwa ajili ya Benyamini, kwa sababu BWANA alikuwa amefanya pengo katika hizo kabila za Israeli.

16. Ndipo hao wazee wa huo mkutano walisema, Je! Tufanyeje ili tuwapatie wake hao waliosalia, kwa kuwa wanawake wameangamizwa katika Benyamini?

17. Wakasema, Lazima kuwa urithi kwa hao wa Benyamini waliopona, isiwe kabila kufutika katika Israeli.

18. Lakini sisi hatuwezi kuwaoza binti zetu kwa maana wana wa Israeli walikuwa wameapa, wakisema, Na alaaniwe huyo atakayempa Benyamini mke.

19. Kisha wakasema, Angalieni, iko sikukuu ya BWANA mwaka baada ya mwaka katika Shilo, ulioko upande kaskazini wa Betheli, upande wa mashariki wa hiyo njia kuu iendeayo kutoka Betheli kwenda Shekemu, nao ni upande wa kusini wa Lebona.

20. Basi wakawaagiza hao wana wa Benyamini wakisema, Haya, endeni, mkaotee katika mashamba ya mizabibu,

21. mkaangalie, kisha tazameni, kwamba hao binti za Shilo watoka ili wacheze katika hiyo michezo, basi tokeni ninyi mizabibuni, nanyi kila mtu na amshike mkewe katika hao binti za Shilo, kisha rudini nchi ya Benyamini.

Amu. 21