6. Basi nikamtwaa huyo suria yangu, na kumkata vipande, na kumpeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli; kwa sababu wametenda maovu makuu na upumbavu katika Israeli.
7. Angalieni, ninyi wana wa Israeli nyote, sasa toeni maneno na mashauri yenu.
8. Basi watu hao wote waliinuka kama mtu mmoja, wakisema, Hatutakwenda, hata mmoja, hemani kwake, wala hatutaondoka, hata mmoja, kwenda nyumbani kwake.
9. Lakini jambo tutakalowatenda watu wa Gibea ni hili; tutakwea kwa kura kwenda kuupiga;
10. nasi tutatwaa watu kumi katika mia katika kabila zote za Israeli, na watu mia katika elfu, na watu elfu katika elfu kumi, ili waende kuwatwalia watu vyakula, ili kwamba, hapo watakapofika Gibea ya Benyamini wapate kutenda mfano wa upumbavu huo wote walioutenda wao katika Israeli.
11. Basi waume wote wa Israeli walikutana pamoja juu ya mji huo, walikuwa wanashikamana pamoja kama mtu mmoja.
12. Kisha kabila za Israeli wakatuma watu waende katika kabila yote ya Benyamini, wakasema, Je! Ni uovu gani huu uliokuwa kati yenu?
13. Basi sasa watoeni watu hao, hao mabaradhuli walio katika Gibea, ili kwamba tupate kuwaua, na kuuondoa uovu katika Israeli. Lakini Benyamini hawakukubali kuisikia sauti ya ndugu zao wana wa Israeli.
14. Lakini wana wa Benyamini wakakutanika huko Gibea kutoka katika miji yao, ili watoke kwenda kupiga vita juu ya wana wa Israeli.
15. Hao wana wa Benyamini walihesabiwa siku ile kutoka hiyo miji, watu waume ishirini na sita elfu waliotumia upanga, zaidi ya hao waliokaa Gibea, ambao walihesabiwa watu wateule mia saba.
16. Katika watu hao wote walikuwako watu waume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa teo, wala asikose.