39. Nao watu wa Israeli walipogeuka katika vile vita, Benyamini naye akaanza kupiga na kuwaua watu wa Israeli kama watu thelathini; kwani walisema, Hakika yetu wamepigwa mbele yetu, vile vile kama katika vile vita vya kwanza.
40. Lakini hapo hilo wingu lilipoanza kupanda kutoka katika mji, kama nguzo ya moshi, ndipo Wabenyamini wakaangalia nyuma, na tazama, huo mji mzima ulikuwa wapaa juu katika moshi kwenda mbinguni.
41. Ndipo watu wa Israeli wakageuka, na watu wa Benyamini walisitushwa; kwa kuwa waliona ya kwamba wamefikiliwa na uovu.
42. Kwa hiyo wakageuza maungo yao mbele ya wana wa Israeli kuelekea njia ya kwenda nyikani; lakini vile vita vikawaandamia kwa kasi; na hao waliotoka katika ile miji wakawaangamiza katikati yake.
43. Waliwazingira Wabenyamini pande zote na kuwafukuza, na kuwakanyaga-kanyaga hapo walipopumzika, hata kufikilia Gibea upande wa maawio ya jua.
44. Wakaanguka watu wa Benyamini watu kumi na nane elfu, hao wote walikuwa ni watu waume mashujaa.
45. Kisha wakageuka na kukimbia upande wa nyika hata kulifikilia jabali la Rimoni; nao wakaokota katika watu hao katika njia kuu watu waume elfu tano; wakawaandamia kwa kasi mpaka Gidomu, nako wakawapiga wengine wao watu elfu mbili.
46. Basi jumla ya watu wa Benyamini walioanguka siku ile walikuwa ni watu ishirini na tano elfu waliokuwa wanatumia upanga; wote hao walikuwa ni watu mashujaa.
47. Lakini watu waume mia sita wakageuka, wakakimbia upande wa nyikani mpaka jabali la Rimoni, wakakaa kwenye hilo jabali la Rimoni muda wa miezi minne.
48. Kisha watu wa Israeli wakageuka tena kuwaendea wana wa Benyamini, wakawapiga kwa makali ya upanga, huo mji mzima, na hao wanyama wa mji, na kila kitu walichokiona; tena miji yote waliyoiona wakaitia moto.