5. Kisha ilikuwa siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, naye akaondoka ili aende zake; baba yake huyo mwanamke akamwambia mkwewe, Tuza moyo wako, ule chakula kidogo, kisha baadaye mtakwenda zenu.
6. Basi wakaketi, wakala na kunywa wote wawili pamoja; kisha baba yake mwanamke akamwambia huyo mtu, Uwe radhi, tafadhali, ukae usiku kucha, na moyo wako na ufurahi.
7. Yule mtu akainuka ili aondoke; lakini mkwewe akamsihi-sihi, naye akalala kuko tena.
8. Basi akaamka asubuhi na mapema siku ya tano ili aende zake; na baba yake mwanamke akasema, Tuza moyo wako, tafadhali, ukae hata jua lipinduke; nao wakala chakula wote wawili.
9. Kisha hapo mtu huyo alipoinuka ili aende zake, yeye na suria yake, na mtumishi wake, huyo mkwewe, baba yake mwanamke, akamwambia, Tazama mchana wakaribia jioni, tafadhali kaa usiku kucha; tazama mchana wakaribia mwisho wake, lala hapa, ili moyo wako ufurahi; hata kesho uende zako asubuhi na mapema, ili upate kwenda kwenu.
10. Lakini huyo mtu hakukubali kukaa usiku huo, ila akainuka, akaenda zake, akafika mkabala wa Yebusi (huo ndio Yerusalemu); nao walikuwako pamoja naye punda wawili waliotandikwa; suria yake naye alikuwa pamoja naye.
11. Basi hapo walipokuwa karibu na Yebusi, mchana ulikuwa umeendelea mno; yule mtumishi akamwambia bwana wake, Haya, tafadhali, tugeuke kando na kuingia mji huu wa Wayebusi, tulale humu.
12. Bwana wake akamwambia, Hatutageuka sisi kuingia mji wa wageni, ambao si wa wana wa Israeli; lakini tutapita mpaka Gibea.
13. Kisha akamwambia mtumishi wake, Haya, tuifikilie miji hii mmojawapo nasi tutalala katika Gibea au katika Rama.