14. Basi wakashika njia kwenda zao mbele; jua likawachwea walipokuwa karibu na Gibea, ambao ni mji wa Benyamini.
15. Wakageuka huko, wapate kuingia na kulala katika Gibea; akaingia ndani, akaketi katika njia kuu ya mji; kwa kuwa hapakuwa na mtu awaye yote aliyewakaribisha nyumbani kwake kulala.
16. Kisha, tazama, akatokea mtu mume mzee, atoka kazini kwake shambani, wakati wa jioni; mtu huyo alikuwa ni wa ile nchi ya vilima vilima ya Efraimu, naye alikuwa anakaa katika Gibea hali ya ugeni lakini wenyeji wa mahali hapo walikuwa Wabenyamini.
17. Naye alipovua macho yake, akamwona huyo mtu msafiri katika njia kuu ya mji; huyo mzee akamwuliza, Waenda wapi wewe? Nawe watoka wapi?
18. Akamwambia, Sisi twapita hapa kutoka Bethlehemu-yuda, twaenda huko upande wa mbali wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu; ndiko nilikotoka nami nilikwenda Bethlehemu-yuda; nami sasa naiendea nyumba ya BWANA wala hapana mtu anikaribishaye nyumbani mwake.
19. Walakini nyasi tunazo, na chakula cha hawa punda zetu; mkate pia tunao na divai kwa mimi na huyu kijakazi wako, na kwa huyu kijana aliye pamoja nasi watumishi wako; hapana uhitaji wa kitu cho chote.